Sisi, wanawake wa vijijini ambao tunasimama kama wazalishaji wakuu wa chakula kwa idadi kubwa ya watu duniani, tunalazimika kuangazia changamoto zinazotukabil ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ardhi na njaa. Wanawake wa vijijini wana mchango mkubwa sana katika sekta ya kilimo, wakichangia kwa kiasi kikubwa usalama wa chakula duniani na kaya. Sisi ni walinzi thabiti wa mbegu za asili, tukihifadhi vizazi vya urithi wa kilimo na bayoanuwai. Kutokana na ujuzi na maarifa yetu ya kuendeleza maarifa kwa vizazi, tunalinda mbegu za asili ambazo ni stahimilivu, tofauti tofauti, na zinazoendana na mifumo ikolojia ya mahali hapo. Mbegu hizi zinawakilisha kiini cha kilimo endelevu, kinachojumuisha kiungo muhimu kwa maisha yetu ya nyuma ya kilimo na mustakabali endelevu. Sisi ni uti wa mgongo katika jamii zetu, tukifanya kazi bila kuchoka katika mashamba ikiwa ni pamoja na mashamba madogo na kuzalisha chakula ambacho kinalisha sio tu wakazi wa eneo hilo bali pia kufikia meza duniani kote.
Kwa masikitiko, tunajikuta tukikumbana na hali mbaya ya kutokuwa na ardhi, hali inayo pelekea kukosa haki muhimu ya kuzalisha na kumiliki ardhi tunayofanyia kazi na kuendeleza mzunguko wa umaskini na kuwaacha wanawake wa vijijini wakiwa wametumbukia katika mapambano yasiyokwisha ili kujikimu na kuhudumia familia zetu. Zaidi ya hayo, pamoja na jukumu letu muhimu katika uzalishaji wa chakula, idadi ya kushangaza ya wanawake wa vijijini na familia zetu tunakabiliwa na njaa na utapiamlo unaosababisha hali mbaya kama vile kujiua kwani hatuwezi kujilisha. Tofauti hii ya wazi kati ya jukumu muhimu tunalobeba katika kulisha ulimwengu na uhaba wetu wa chakula haikubaliki na inasumbua sana.
Mifumo hii ya chakula iliyovunjika inazidisha changamoto kwetu, huku ikikuza vikwazo vinavyowakabili wanawake wa vijijini katika jamii na kukosa au kushindwa kufikia rasilimali ardhi na maji:
1. Ukosefu wa usalama wa chakula kutokana na mifumo ya chakula Iliyoharibika: Mifumo ya chakula isiyofaa, isiyo na usawa, na isiyoweza kuhimili mazingira inachangia kuongezeka kwa uhaba wa chakula miongoni mwa wanawake wa vijijini. Dosari zilizopo katika njia za usambazaji, mbinu zisizostahili katika masoko na kukosekana kwa mifumo wezeshi kunasababisha kupungua kwa upatikanaji wa chakula chenye lishe kwa ajili yetu na familia zetu. Mifumo ya vyakula ya ndani inaharibiwa ili masoko ya kimataifa yaweze kupata soko ikiwa ni pamoja na vijiji vya pembezoni.
2. Ukosefu wa Upatikanaji wa Ardhi na Maji: Wanawake wengi wa vijijini wanatatizika kupata na kudhibiti rasilimali ardhi na maji, muhimu kwa kilimo endelevu. Upatikanaji mdogo wa ardhi ya umwagiliaji na vyanzo vya maji vinavyotegemewa hupunguza uwezo wetu wa kuzalisha chakula cha kutosha na hivyo kuendeleza mzunguko wa njaa na umaskini.
3. Uharibifu wa Mazingira unaathiri uzalishaji wa chakula: Changamoto za kimazingira kama vile mabadiliko ya tabia nchi, ukataji miti, uharibifu wa udongo, na upotevu wa bayoanuwai huathiri sana mfumo wetu wa ikolojia na hivyo kuongeza mapambano katika uzalishaji wa chakula cha kutosha kukidhi familia na jamii zetu. Uharibifu wa bayoanuwai ikiwa ni pamoja na kupotea kwa aina mbalimbali za mimea na wanyama, huvuruga mifumo ya ikolojia, huvuruga mzunguko wa uchavushaji, na kudhoofisha ustahimilivu wa asili wa mifumo yetu ya kilimo na hivyo kuwa tishio la dharura kwa usalama wetu wa chakula. Kama wanawake wa vijijini, tunashuhudia moja kwa moja matokeo makubwa ya athari hizi za kiikolojia juu ya uwezo wetu katika kuzalisha mazao anuwai na lishe, tukisisitiza haja ya kuwa na njia endelevu za kilimo zinazozingatia bayoanuwai.
4. Sera na mgao wa rasilimali usio na usawa: Sera zisizotoa kipaumbele kwa mahitaji ya wanawake wa vijijini na ukosefu wa mgao sawa wa rasilimali zilnatuweka pembeni zaidi na hivyo kukwamisha uwezo wetu katika kuongeza tija kwa kilimo na katika kuboresha hali ya maisha.
5. Ukosefu wa mifumo ya kifedha ya kuwezesha njia mbadala madhubuti kama vile kilimo ikolojia na badala yake ruzuku inaelekezwa kwa makampuni ya kimataifa kusambaza mbolea/viuatilifu vya kikemikali na mbegu za viini tete.
Tunatoa wito kwa serikali, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa kushughulikia masuala haya muhimu:
- MAREKEBISHO YA SERA NA SHERIA SAIDIZI: Serikali lazima zitunge na kutekeleza sera zinazokuza haki za ardhi kwa wanawake wa vijijini, kuhakikisha upatikanaji na umiliki sawa. Sheria pia inapaswa kushughulikia soko lenye manufaa sawa na haki na kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo.
- KILIMO ENDELEVU NA MBINU STAHIMILIVU KWA MABADILIKO YA TABIA NCHI: Kuhimiza na kuendeleza mbinu endelevu za kilimo-ikolojia na mbinu za kilimo zinazostahimili mabadiliko ya tabia nchi ili kupunguza changamoto za kimazingira na kuimarisha usalama wa chakula kwa wanawake wa vijijini.
Sisi ni walinzi wa ardhi, uhai, mbegu na upatikanaji wa riziki. Ustahimilivu wetu na uamuzi wetu hauna kikomo. Ni wakati wa kujitoa kwa pamoja kushughulikia changamoto hizi na kujenga ulimwengu ambapo wanawake wa vijijini wanapata ardhi, maji, na rasilimali muhimu kwa maisha yenye heshima na mustakabali usio na njaa.